Mwanafunzi auawa na majambazi Kenya

Image caption Mwanafunzi akifungasha virago tayari kuondoka shuleni

Mwanafunzi mmoja nchini Kenya ameuawa kwa kupigwa na watu wanaoshukiwa kuwa majambazi ambao walivamia shule moja viungani mwa mji mkuu Nairobi.

Mwanafunzi huyo na wenziwe walikuwa wamelala kwenye bweni lao katika Shule ya St. Charles Mutego iliyoko katika kitongoji cha Dagoreti, Magharibi mwa Nairobi.

Wanafunzi wengine 50 walijeruhiwa.

Inaarifiwa watu hao walivamia shule hiyo na kuzima taa na baadaye kuvunja madirisha ya vioo pamoja na magari yaliyokuwa yameegeshwa shuleni hapo na kisha kuwapiga wanafunzi waliokuwa wamelala.

Mkurugenzi mkuu wa shule hiyo Charles Niyamote ameiambia BBC kuwa kiini cha mashambulizi haya huenda ikawa ni wivu, kwa sababu wanaona shule hiyo ina watoto wengi. Walipokuwa wakitekeleza uhalifu huo, waliwaambia watoto hao waitoroke shule hii.''

Polisi walidhibitisha tukio hilo lakini walikataa kutoa taarifa hadi watakapokamilisha uchunguzi wao. Hakuna mshukiwa aliyekamatwa hadi kufikia sasa.

Kwa sasa shule hiyo imefungwa kwa muda wa wiki moja wakati polisi wakiendelea na uchunguzi wa kina.

Visa vya ukosefu wa usalama vimeongezeka katika mji wa Nairobi na maeneo mengine ya Kenya katika siku za hivi karibuni, lakini si jambo la kawaida kwa wanafunzi kuvamiwa kwa njia hii wakiwa shuleni.