Rwanda kudhibiti mali ya 'wapinzani'

Image caption Rais wa Rwanda Paul Kagame

Bunge la Rwanda limepitisha sheria tata inayoruhusu serikali kudhibiti mali ya raia wa nchi hiyo ambao hawaishi nchi humo.

Wakosoaji wa serikali hata hivyo wanasema kuwa hii ni njama ya serikali kuchukua mali ya watu wanaoonekana kuwa wapinzani wakuu wa serikali ya Rais Paul Kagame.

Wizara ya sheria ambayo ilipendekeza mswada huo, bungeni ilisema kuwa sheria yenyewe inanuia kuzuia migogoro yoyote inayotokana na mali ya watu.

Ushindani wa kumiliki ardhi nchini Rwanda , umesababisha mvutano na hata umetajwa kuwa moja ya mambo yaliyosababisha mauaji ya kimbari mwaka 1994.

Serikali inasema kuwa sheria hiyo italenga tu mali ambayo wamiliki wao hawajulikani au wamefariki bila ya watu kurithi mali hiyo.

Hata hivyo mgogoro umezuka kuhusu serikali kutaka kudhibiti mali ya mmoja wa matajiri wakubwa wa nchi hiyo Tribert Rujugiro, ambaye sasa anaishi uhamishoni.

Wakosoaji wanasema kuwa mpango huo unalenga mali ya tajiri huyo ikiwemo jengo kubwa la kibiashara ambalo limekuwa likidhibitiwa na serikali tangu mwaka jana.

Mfanyabiashara huyo ambaye alikuwa wakati mmoja mshirika mkubwa wa chama tawala RPF alikosana na Rais Kagame baada ya kumwambia kuwa haheshimu sheria pamoja na kumkosoa kwa kuingilia hukumu zinazotolewa na mahakama

Serikali imekanusha madai hayo ikisema kuwa haina nia ya kuchukua mali ya watu bila kuelezea ni kwa muda gani.

Wizara ya sheria inasema kuwa zaidi ya watu 700 wataathirika.

Kwa sasa mswada huo umepitishwa na bunge na kilichosalia ni kupigiwa kura na baraza la Senate kabla ya kutiwa saini na Rais Kagame.