Sudan.K: Duru ya pili ya mazungumzo

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Pande zinazozozana zinasema kuwa mapigano yamesitishwa ingawa taarifa zinasema sivyo

Duru ya pili ya mazungumzo ya kusitisha vita nchini Sudan Kusini kati ya Waasi na serikali yataanza tena leo mjini Adis Ababa Ethiopia.

Pande hizo mbili zilitia saini makubaliano ya kusitisha mapigano mapema mwezi uliopita baada ya shinikizo kutoka jamii ya kimataifa.

Pande hizo zimekua zikisisitiza kwamba zinatii makubaliano hayo licha ya kwamba bado mapigano yanaendelea katika baadhi ya maeneo ya Sudan Kusini.

Mkutano wa leo hata hivyo hauna ajenda kuu kuhusu kitakachozungumziwa huku kukiwa na taarifa za mapigano kuendelea licha ya mkataba wa kuyasitisha kutiwa saini.

Maelfu wamelazimika kutororoka makwao huku wakihitaji msaada wa dhahura wa kibinadamu.

Athari za mapigano hayo kwa karibu miezi miwili zimedhihirika miongoni mwa wananchi, maelfu wameuwa na wengine zaidi ya lakini nane kuachwa bila makao.

Pande zinazozozana zimetuhumiwa kwa kupuuza mkataba wa amani kama walivyokubaliana mwezi jana. Shirika la kikanda la IGAD, tayari limetuma kikundi cha maafisa wakuu kuchunguza hali na kuhakikisha kuwa pande zote zinazozozana zinatekeleza mkataba wa amani.

Lakini wanajeshi wa Salva Kiir na waasi wanaomuunga mkono aliyekuwa makamu wake Riek Machar, wamekuwa wakipigana na kutuhumiana hadharani, kabla ya mkutano wa pili wa mazungumzo ya amani.

Ghasia zilizuka Disemba mwaka jana nchini Sudan Kusini na kusababisha ghasia kati ya makundi hasimu jeshini. Umoja wa amataifa unasema kuwa takriban watu milioni 3.7 wanahitaji msaada wa chakula.