Awamu ya pili ya mazungumzo ya Syria

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Syria Lakhtar Brahimi

Awamu ya pili ya mazungumzo kati ya makundi ya upinzani katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria yameanza rasmi mjini Geneva.

Hatua hiyo inajiri baada ya awamu ya kwanza ya mazungumzo hayo kuvunjika juma moja lililopita huku pande zote mbili zikikosa kupiga hatua kuhusu kusitishwa kwa vita hivyo.

Huku mazungumzo ya amani yakianza tena, juhudi zinafanyika kuwahamisha raia zaidi kutoka katika sehemu za mji uliotekwa na waasi, Homs na kuwapa msaada wa chakula wale ambao bado wamekwama mjini humo.

Zaidi ya watu 600 walisindikizwa kutoka mjini humo siku ya Jumapili.

Taarifa za kusitishwa vita kwa siku tatu ili msaada uweze kutolewa,hazijathibitishwa rasmi, lakini pande zote mbili zinaoenekana kuendelea na shughuli kama kawaida na kuruhusu msaada kuingizwa mjini Homs.

Shirika la msalaba mwekundu nchini Syria, limesema kuwa linajaribu kufungua njia ya kupitishia msaada kwa waathiriwa wa vita.

Wakati huohuo, wafungwa 20 wameripotiwa kufariki katika jela rasmi mjini Aleppo baada ya waasi kuzuia msaada wa chakula na dawa kuingizwa mjini humo.

Huku hayo yakijiri, serikali ya Syria imekiri kuwa baadhi ya watu waliohamishwa toka mji wa Homs hapo jana wamekamatwa na kuzuiliwa.

Msemaji wa wizara ya habari ya taifa hilo Daktari Bassam Abu Abdullah ameiambia BBC kuwa watu 103 anaowataja kama wapiganaji wamezuiliwa na walinda usalama lakini anadai kuwa waliachiliwa baadaye.

Anasema kuwa serikali ilitaka kujua watu waliookolewa toka mji huo.

Lakini duru za habari zasema kuwa watu hao bado hawajaachiliwa kwani wangali wamezuiliwa pamoja na jamii zao.

Taarifa toka mji wa Homs zasema kuwa muafaka wa siku tatu wa kukomesha mapigano uliomalizika hapo jana jioni ulishuhudia milipuko mibaya usiku wa kuamkia leo lakini kufikia leo mchana hali imetulia kiasi.