Waasi na serikali kusitisha mapigano Syria

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Raia wa Syria waliojeruhiwa mjini Homs

Umoja wa mataifa unasema pande zote zinazohusika na mzozo mjini Homs nchini Syria, zimeafikiana kuongeza muda wa kusitisha mapigano kwa siku tatu zaidi ili watu zaidi ya elfu tatu waliokuwa wamekwama kwenye mapigano wakiokolewa kutoka mji huo leo.

Mkuu wa kitengo cha misaada ya kibinadamu katika Umoja wa Mataifa , Valerie Amos, ameeleza masikitiko yake kuhusu vile mkataba wa awali wa kusitisha mapigano ulipuuzwa hali iliyosababisha watu 11 .

Angalau wakati huu hakukuwa na mashambulizi mjini Homs lakini kwengineko katika mji mkuu wa Damascus, makombora yamevurumishwa na kusababisha kusitishwa kwa zoezi la kutoa misaada ya chakula.

Walionusuriwa kutoka maeneo ya mashambulizi hasa wanawake watoto na wazeee, wakibubujikwa na machozi baadhi wakieleza jinsi walivyokuwa wakila nyasi baada ya kukosa chakula.

Yacoub el Hillo ambaye ni mratibu wa operation hiyo ya Umoja wa Mataifa huko Syiria anasema bado kuna kazi nzito ya kufanya kuwasaidia raia wa Syira wanaoathirika na vita hivyo kila uchao.

''Yapo mengi ya kujifunza katika operaion tunayoendelea nayo mjini Homs, mafanikio kwa sasa ni machache ukilinganisha na lile linalopaswa kufanywa. Jitihada zaidi zahitajika kukabiliana na hali hii.'' Amesema Yacoub el Hillo.

Wadadisi wanasema mkataba wa amani pekee ndio utatoa mwanya wa kushughulikia janga la kibinadamu linalowakumba raia wa Syria, lakini kwa sasa hilo limebakia kuwa ndoto.

Upinzani unataka serikali ikubali kwa maandashi sharti la kuwekwa kwa halmashauri ya serikali ya mpito.

Lakini rais Bashar al-Assad amekataa katakata kungatuka madarakani.

Duru ya kwanza ya majadiliano iliishia kutupiana maneno na pande hizo mbili hazijakutana ana kwa ana.

Vita vya Syria, vimesababisha vifo vya takriban watu laki moja tangu vianze 2011 na zaidi ya watu millioni 9 unusu wameyatoroka makaazi yao.