Bensouda:Sikabiliwi na shinikizo zozote

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Fatou Bensouda akiongea na wandishi wa habari

Kiongozi wa mashitaka katika mahakama ya kimataifa ya ICC,Fatou Bensouda, amekanusha madai kuwa anakabiliwa na shinikizo za kisiasa kufutilia mbali kesi dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta na makamu wake William Ruto.

Bensouda katika taarifa yake kwa vyombo vya habari alisema kuwa hana shinikizo zozote kutoka kwa aliyekuwa mkuu wa mashitaka katika mahakama hiyo Luis Moreno Ocampo, kuwa afutilie mbali kesi hizo.

Amesema kuwa uamuzi na vitendo vya mwendesha mkuu wa mashitaka kuhusu kesi huzingatia sheria. Pia amesema kuwa uamuzi wake kuendelea na kesi inategemea ushahidi alionao kuhusu kesi hiyo.

Ocampo ndiye aliyewashitaki Uhuru na Ruto pamoja na viongozi wengine wa kisiasa Kenya, ICC kuwa washukiwa wakuu wa ghasia za baada ya uchaguzi mkuu nchini Kenya mwaka 2007/08.

Aidha Ocampo alinukuliwa mwishoni mwa wiki akisema kuwa kushitakiwa kwa Kenyatta na Ruto, kulitokana na shinikizo za mabalozi wa kigeni kuwazuia wawili hao kuwania urais mwaka jana.

Hata hivyo baada ya taarifa hiyo kuenea Ocampo alibadili kwa kusema kuwa tamko la mabalozi halikuwa na uhusiano wowote na makosa ya jinai yaliyokuwa yanawakabili viongozi hao wawili.

Kwake njia ambayo angetumia kufanya kuwazuia Ruto na Kenyatta kugombea kisiasa ilikuwa kuwapeleka wawili hao katika mahakama ya Hague.

Kesi dhidi ya Kenyatta na Uhuru imekuwa ikikumbwa na changamoto si haba huku baadhi ya mashahidi wakijiondoa wakisema kuwa walishurutishwa kwenda kutoa ushahidi dhidi ya wawili hao huku wakiahidiwa mambo mazuru ikiwa watakubali kufanya hivyo.

Kwa sasa mahakama ya ICC inajadili kuhusu mustakabali wa kesi ya Kenyatta ambayo mwendesha mkuu wa mashitaka alitaka isitishwe kwa muda kutokana na kukosa ushahidi wa kutosha.

Mahakama ya ICC itaamua katika muda wa wiki mbili zijazo ikiwa kesi hiyo itaendelea au kusitishwa kwa muda usiojulikana au hata kutupiliwa mbali.