Wakazi wa Homs Syria wapata afueni

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wakazi wa Homs wanaishi katika mazingira duni sana

Mwandishi wa BBC katika mji uliozungukwa Homs nchini Syria anasema magari mawili yaliobeba chakula yamefika katika mji huo.

Kuna mabasi pia karibu na eneo hilo yalio tayari kuwabeba na kuwaondosha mjini humo.

Makubaliano ya kusitisha mapigano kwa muda yanatarajiwa kumalizika leo lakini gavana wa Homs amesema kwamba atajaribu kuendelea kusitisha mapigano kwa muda mrefu iwezekanavyo, ili kuruhusu kuondolewa raia zaidi walio hatarini.

Mpaka sasa ni watu 1200 wameondoka mjini humo.

Baadhi ya wafuasi wa serikali wamekasirishwa kuhusu uwezekano wa kutoweka kwa wapinzani waliojihami huku makundi ya upinzani yakiwa na hasira kwamba vijana wanaoondoka Homs wanakaguliwa na maafisa wa serikali.

Wakati huo huo wakimbizi nchini Syria wanaripotiwa kumiminika katika mji wa Lebanon wa Arsal kutokana na uvumi wa uwezekano wa kuzuka shambulio la jeshi la serikali Syria katika mji ulio karibu wa Yabroud.

Mwandishi wa BBC katika eneo hilo, ameambiwa na maafisa katika eneo hilo la Arsal kwamba familia 170 zimevuka mpaka kabla ya hapo jana Jumanne na kwamba wengine zaidi wanazidi kuwasili.

Mwandishi wa BBC anasema shambulio la kijeshi dhidi ya mji wa Yabroud unaosalia kuwa ngome ya waasi, huenda likasababisha maelfu ya raia wa Syria kuvuka mpaka na kuingia Arsal, eneo ambalo tayari lina idadi kubwa ya wakimbizi kutoka Syria.