Uganda yaambia Tullow haitaki masharti

Image caption Mashine za kampuni ya kuchimba mafuta ya Tullow nchini Uganda

Serikali ya Uganda imesema kuwa haitashurutishwa kufanya kile ambacho kampuni za mafuta zinataka.

Hapo jana kampuni ya kuchimba mafuta ya Tullow Oil moja ya kampuni tatu zinazoendesha shughuli za kuchimba mafuta nchini humo, imesema kuwa huenda ikauza sehemu ya hisa zake kwa sababu nchi jirani ya Kenya imetoa mazingira mazuri ya kazi kwa kampuni hiyo kuliko Uganda.

Serikali ya Uganda imejikuta katika mzozo na kampuni ya Tullow Oil na washirika wake wawili,Total na CNOOC ya China kuhusu namna ya kuuza mafuta ghafi.

''Kampuni hizo ziko huru kununua na kuuza bidhaa zake nchini Uganda lakini serikali ina haki ya kujali maslahi ya raia wake kwanza'', kwa mujibu wa msemaji wa wizara ya afya, Bukenya Matovu.

Alielezea kushtushwa na matamshi ya kampuni ya Tullow, baada ya kutia saini mkataba wa maelewano na serikali kuhusu uzalishaji wa mafuta.

Pande hizo mbili, zimekubaliana kuhusu ikiwa Uganda, inapaswa kujenga kiwanda cha kusafisha mafuta.

Maafisa wanasema, ni muhimu kwa Uganda kuongeza thamani mafuta yake ghafi lakini kampuni ya Tullow imesema kuwa kuuza mafuta ghafi katika nchi za kigeni ina faida zaidi kuliko kuyauza nchini humo.

Makubaliano ya wiki jana kati ya pande hizo mbili, yatahakikisha kutekelezwa kwa mipango hiyo.

Aidha kampuni hiyo inatarajia kuanza kuuza mafuta nchini Kenya mwaka 2016.