US yapinga kuachiliwa wafungwa Afghanistan

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Mfungwa katika gereza ya Bagram

Maafisa nchini Afghanistan wamewaachiwa wafungwa 65, wengi wao ambao Marekani inasema walihusika na mauaji ya walinda amani wa kimataifa na wanajeshi wa Afghanistan.

Msemaji wa waziri wa ulinzi nchini humo Mohammad Zahir Azimi, alithibitisha taarifa hizo ingawa Marekani inasisitiza kuwa ina ushahidi wa kutosha dhidi ya wafunga hao wanaohusishwa na milipuko na mashambulizi mengine.

Lakini serikali inasema kuwa hakuna ushahidi wa kutosha dhidi ya wafungwa hao.

Rais Karzai, ameitaja jela ya Bagram kama kitovu cha Taliban ambako wafungwa wanaondoka jela wakiwa na misimamo mikali zaidi dhidi ya serikali.

Karzai amesema kuwa wafungwa hao waliteswa na kutiliwa kasumba ya kuichukua nchi yao.

Balozi wa Marekani mjini Kabul amesema kuwa uamuzi wa kuwaachilia wafungwa hao ni wa kusikitisha mno.

Ameitaka serikali kuhakikisha kuwa walioachiliwa hawatatenda uhalifu

Duru zinasema kuwa kuachiliwa kwa wafungwa hao ni ishara ya kudorora kwa uhusiano kati ya majeshi ya Marekani na Rais wa Afghanistan Hamid Karzai.