Wadau watetea wanyamapori London

Haki miliki ya picha AP
Image caption China ndio mhalifu mkubwa katika biashara ya pembe za Ndovu na Vifaru

Wahifadhi wakuu wa mazingira kutoka kote duniani wanakutana mjini London Uingereza kubuni mikakati ya kukomesha uwindanji haramu wa wanyamapori walio katika hatari ya kuangamia.

Moja ya malengo ya wadau hao ni kumulika changamoto wanazokabiliwa nazo wanyama pori kama Vifaru na Ndovu ambao huenda wakaangamia katika kipindi cha miaka 15 ikiwa uwandaji haramu hautakomeshwa.

Wanaharakati wanasema kuwa soko la pembe za wanyama hao linachochewa na biashara nchini China.

Mkuu wa shirika la kulinda wanyamapori nchini Kenya, Paula Kahumbu ameambia BBC kuwa madhumuni ya kongamano hilo ni kuona kuwa China inaharamisha biashara ya pembe za Ndovu na vifaru.

Kahumbu anasema kuwa biashara haramu ya wanyamapori zisingekuwa zinafanyika ikiwa serikali za Kenya, Uganda na Tanzania zingechukua hatua kali.

Alisisitiza kuwa ufisadi unaruhusu watu kusafirisha makonteina makubwa makubwa yenye pembe za Ndovu na Vifaru kutoka Afrika. Pia ametoa wito kwa China kuharamisha biashara ya Pembe za Ndovu.

Wajumbe kutoka nchi 46 na mashirika 11 ya kimataifa, watahudhuria kongamano hilo, wakiwemo marais kadhaa wa nchi za Afrika ambazo ziomejitolea kupambana na uwindaji haramu wa Ndovu na Vifaru.

Moja ya anchi ambazo zinatoa adhabu kali kwa watakaopatikana na hatia ya kujihusisha na biashara haramu ya pembe za Ndovu au Vifaru, ni Kenya.