Filamu ipi itang'aa kwenye Baftas?

Haki miliki ya picha AP
Image caption Filamu ya Gravity inapigiwa upatu kupata tuzo nyingi

Judi Dench, Sandra Bullock, Tom Hanks na Leonardo DiCaprio watakuwa miongoni mwa waigizaji mahiri kuhudhuria hafla ya tuzo za filamu za Baftas nchini Uingereza Jumapili.

Filamu kuhusu anga za juu zaidi, Gravity iko kifua mbele ikiwa imeteuliwa katika vitengo 11 pamoja na filamu nyingine ambayo imekuwa ikigonga vichwa vya habari kuanzia mwaka huu '12 Years a Slave'. Filamu hiyo inapigiwa upatu kupata tuzo kadhaa.

Baftas ni tuzo kubwa zaidi kutolewa kwa sekta ya filamu duniani kabla ya tuzo za Oscars tarehe 2 mwezi Machi.

Mwanamfalme wa Uingerezea Prince William,atahudhuria hafla hiyo katika jumba la kifahari la London Royal Opera House.

Filamu iliyozungumziwa sana mwaka huu '12 Years a Slave' yake mtengeza filamu Muingereza Steve McQueen, ambayo inahusu Mmarekani mmoja aliyeuzwa utumwani baada ya kutekwa nyara, imepata uteuzi katika vitengo 10 ikiwemo, filamu bora zaidi , mtengeza filamu bora na muigizaji bora kumwendea Chiwetel Ejiofor.

Wadadisi wanasema kuwa filamu hiyo iliyowasikitisha wengi kuhusu mada yake, huenda ikashinda tuzo 5.

Filamu nyingine iliyofanya vyema na hata kupigwa marufuku nchini Kenya na kwingineko duniani kwa matumizi ya lugha chafu,American Hustle, imepata uteuzi mara kumi na waigizaji wake wakuu Amy Adams, Christian Bale, Bradley Cooper na Jennifer Lawrence pia wamepigiwa upatu kupata tuzo.

Filamu nyingine ambazo zinapigiwa upatu kupata tuzo ni, filamu kuhusu uharamia Somalia ,Captain Phillips na Philomena, ambayo inahusu mwanamke anayemtafuta mwanawe ambaye alilazimishwa kumtoa kwa watu waliotaka kumuasili yake Judy Dench.

Captain Phillips, imepata uteuzi mara 9. Je unaipigia filamu ipi upatu kushinda Baftas?