Mhamiaji mmoja auawa katika kambi ya PNG

Haki miliki ya picha none
Image caption Wahamiaji haramu wakiwasili kwa mashua nchini Australia

Mkimbizi mmoja ameuawa na wengine zaidi ya 70 wamejeruhiwa kufuatia ghasia zilizozuka katika kituo cha uhamiaji cha Australia kilichoko katika pwani ya Papua New Guinea. Vurugu hizo zinametokea baada ya mahabusu 35 kutoroka kutoka katika kituo hicho kilichoko katika kisiwa cha Manus siku ya Jumapili.

Baada ya siku mbili za vurugu usiku kucha, maafisa wa uhamiaji nchini Australia wanasema kuwa walinzi wamethibiti kituo hicho cha kuwazuilia wahamiaji kilichoko katika kisiwa cha Manus nchini Papua New Guinea.

Mmoja wa watu hao wanaotafuta hifadhi nchini Australia ameuwawa na zaidi ya sabini wamejeruhiwa vibaya. Waziri wa uhamiaji wa Australia, Scott Morrison, ametaja mauaji hayo kama mkasa akisema kuwa usalama umeimarishwa kuhakikisha kuwa hakuna vurugu nyingine itatokea katika kambi hiyo kama ilivyokuwa katika kisiwa cha Nauru bahari ya Pacifi mwaka uliopita ambapo kituo hicho kiliteketezwa.

"Hii ni hali ya kutamausha lakini sio jambo ambalo tulitarajia. Serikali imekuwa ikichukua hatua kuimarisha usalama katika kituo hicho katika majuma ya hivi karibuni. Serikali imepata funzo kutokana na majaribio ya kuharibu vituo vilivyo Nauru ambayo yalifanikiwa na vituo hivyo kuharibiwa kabisa," anasema Scott Morrison.

Makundi ya wakimbizi yanasema kuwa vurugu hizo zilianza wakati watu waliazuiliwa walipata habari kwamba watapewa makao nchini Papua new guinea na wala sio Australia. Wanaharakati wameripoti kwamba mahabusu walishambuliwa na maafisa wa polisi wa Papua New Guinea na wenyeji madai ambayo waziri wa uhamiaji wa Australia ameyakanusha.

"Taarifa yangu mapema hivi leo ilieleza bayana kwamba hapakuwa na polisi wa PNG katika kambi hiyo usiku wa kuamkia leo. Hiyo ndiyo ripoti niliyopewa usiku na hiyo ndio habari niliyonayo. Kwa hivyo madai kwamba polisi wa PNG walikuwa katika kambi hiyo sio sawa kwa mujibu wa taarifa niliyo nayo. G4S imeshauri kwamba hakuna mtu kutoka nje alioyejaribu kuvuruga au kuwashambulia watu walio ndani na kupelekea ua wa seng'enge kukatwa.''

Australia inasisitiza kuwa kambi zake za kuwakagua wakimbizi nje ya Australia katika kusini mwa bahari ya Pacific zinasaidia kukabiliana na idadi kubwa ya watu wanaotafuta hifadhi nchini Australia ambao wanawasili kwa mashua.