Boko Haram bado ni hatari Nigeria

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wapiganaji wa Boko Haram

Taarifa kutoka nchini Nigeria, zinasema kuwa kumekuwa na mashambulizi mabaya sana dhidi ya wakazi wa mji wa mpakani wa Bama, siku moja baada ya msemaji wa Rais kusema kuwa jeshi linashinda vita dhidi ya wapiganaji wa Boko Haram.

Seneta wa jimbo la Borno, Ahmed Zanna ameambia BBC kuwa mashambulizi hayo yaliyotokea Jumatano asubuhi yalidumu kwa masaa 5

Siku ya Jumanne, msemaji wa jeshi Doyin Okupe, alisema kuwa jeshi limeweza kudhibiti hali.

Zaidi ya watu 254 wameuawa mwaka huu pekee na watu wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wa kundi la Boko Haram.

Maelfu wameuawa tangu Boko Haram kuanza vita dhidi ya serikali mwaka 2009.

Taarifa ya bwana Okupe, ilitofautiana na matamshi ya gavana wa jimbo la Borno ambalo ni kitovu cha Boko Haram.

Gavana Kashim Shettima, ametoa wito wa kutaka wanajeshi zaidi na ambao wamejihami vilivyo kupelekwa katika jimbo hilo, kuliko vikosi vya usalama vilivyoko katika jimbo hilo.

Taarifa kuhusu mashambulizi ya leo bado hazitajitokeza lakini wakazi wa eneo hilo wamewasiliana na idhaa ya BBC Hausa kuhusu mashambulizi ya leo.

Mji huo hata hivyo umewahi kushambuliwa katika siku za nyuma.