Gavana wa benki kuu ya Nigeria afutwa

Image caption Lamido Sanusi -aliyekuwa gavana wa benki kuu ya Nigeria

Rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan, amemsimamisha kazi gavana wa benki kuu ya nchi hiyo Lamido Sanusi .

Sanusi analaumiwa na shirika la mafuta nchini humo kwa kutowasilisha mapato ya mafuta ya kima cha mabillioni.

Hata hivyo taarifa ya serikali inasema kuwa Sanusi amesimamishwa kazi kwa kile wanachokiita kuwa maamuzi yake yake yasiyo ya busara .

Bw Sanusi alijipatia umaarufu kwa kupambana na ulanguzi wa fedha katika sekta ya mabenki nchini Nigeria.

Alikuwa ameratibiwa kustaafu mwezi juni.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari kutoka ikulu ya rais, Lamido Sanusi amesimamishwa kazi kama gavana wa benki kuu ya Nigeria, kutokana na kile kilichotajwa kuwa utovu wa nidhamu na sera mbovu za kiuchumi.

Hivi majuzi alisababisha kashfa kubwa ya kisiasa pale ilipoibuka kuwa kulikuwepo na usimamizi mbaya katika secta ya mafuta ambayo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa Nigeria .

Secta ya mafuta, imebainika kuwa imeshindwa kuwasilisha zaidi ya dola bilioni ishirini kwa serikali kutokana na mauzo ya mafuta.

Secta hiyo imejawa na ukiritimba mkubwa na ni moja ya secta ambayo inaongoza katika ufisadi.

Bunge la Nigeria kwa sasa linachunguza madai hayo dhidiya Lamido Sanusi.

Raia wengi wa Nigeria wanahisi kuwa rais Goodluck Jonathan amemuondoa gavana huyo, kwa kuhofia kuwa ufisadi miongoni mwa maafisa wake wakuu utafichuliwa kabla ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwakani.