Ulaya itawabana wanaozua vurugu Ukraine

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Hali bado ni tete Ukraine

Umoja wa Ulaya umekubali kuwawekea vikwazo watu waliohusika katika kuzua vurugu zinazoikabili Ukraine kwa sasa.

Uamuzi huo uliofanyika mjini Brussels, umejiri baada ya makumi kadhaa ya watu kuuwawa mjini Kiev, katika siku ambayo ilishuhudia umwagikaji mkubwa zaidi wa damu nchini Ukraine tangu uhuru zaidi ya miaka ishirini iliyopita.

Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Italia, Emma Bonino, amesema vikwazo hivyo vinavyojumuisha vikwazo vya usafiri na kupiga tanji mali za wahusika, vitawalenga wale waliohusika na mauaji ya waandamanaji.

Ujumbe wa Umoja wa Ulaya mjini Kiev unajaribu kuwapatanisha viongozi wa upinzani na rais Victor Yanukovych ili kuleta amani na pia kushawishi taifa hilo kuandaa mapema uchaguzi uliopangiwa kufanyika mwaka ujao.

Katibu mkuu wa umoja wa mataifa , Ban Ki-moon amesema hali nchini Ukraine ni ya kutamausha.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Walenga shabaha wameshutumiwa kuwauwa waandamanaji.

" Nasikitishwa sana na jinsi mambo yalivyogeuka na kuwa mkasa nchini Ukraine hususan hapo jana ambapo zaidi ya watu mia moja waliuwawa na vurugu hizi zilizozuka upya," amesema bwana Ban.

Bwana Ban ametowa wito kwa pande zote kurejea kwenye meza ya mazungumzo.

"Naendelea kutoa wito kwa wato wanaohusika kukomesha vurugu na kwa mamlaka za ukraine kujiepusha na matumizi ya nguvu kupita kiasi. Nimetamaushwa sana na visa vya matumizi ya silaha miongoni mwa polisi na waandamanaji. Natoa wito kwa pande zote mbili kurejea mara moja katika mazungumzo ya dhati, hii ndio njia ya pekee ya kukomesha umwagikaji wa damu na kufikia suluhu juu ya mzozo wa kiasi, kiusalama na kiuchumi unaozidi kukithiri."

Wito huo umetolewa vile vile na waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa marekani John Kerry ambaye ametaka vurugu kusitishwa nchini Ukraine kukomeshwa akisema kuwa watu wa taifa hilo wanastahili kuwa na hali bora kuliko kile alichokitaja kuwa maafa na mateso yasiyofaa ambayo yameshuhudiwa katika barabara za mji mkuu mkuu wa Kiev.

Haijabainika ni watu wangapi waliouwawa katika vurugu za Alhamisi lakini wizara ya Afya inasema tangu Jumanne, watu sabini wamuewawa na zaidi ya 570 wamejeruhiwa.