Rais Mubage afikisha miaka 90

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Mugabe ametawala Zimbabwe tangu mwaka 1980

Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe amefikisha miaka 90 leo na kuwa rais mkongwe zaidi barani Afrika.

Amekuwa Rais wa Zimbabwe tangu nchi hiyo ijipatie uhuru mwaka 1980.

Hata hivyo sherehe za siku ya kuzaliwa kwake zitafanyika Jumapili huku kukiwa na tetesi kuhusu hali yake mbaya ya kiafya pamopja na mvutano kuhusu uongozi wa chama tawala.

Sherehe hizo zinakisiwa kugharimu dola milioni moja.

Mugabe alichukua mamlaka mwaka 1980 wakati Zimbabwe ilipojinyakulia uhuru kutoka kwa Uingereza na amekuwa akisemekana kuwa mgonjwa sana.

Amekuwa akienda nchini Singapore, kwa ukaguzi wa kimatatibabu mara kadhaa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Taarifa zilifichuliwa mwaka 2008 kuwa Mugabe anaugua Saratani ya tezi kibofu, madai ambayo serikali ilikanusha vikali.

Taarifa hizi ziwe za kweli au za uongo, cha mno ni kwamba kwa sasa Zanu-PF kinajiandaa kwa maisha bila ya Rais Mugabe.

Hata hivyo mnamo siku ya Alhamisi Mugabe alisema hakuna umuhimu wowote wa kuanza kuzungumzia swala la Urithi wakati yeye yungalipo.

"kwa nini swala hili lijadiliwe wakati muda bado? Je muda umewadia wa kulizungumzia?'' alinukuliwa akihoji na gazeti la The Herald nchini Zimbabwe

"uongozi bado upo . Yaani bado nipo,'' alisema Mugabe