Taleban lakiri kuwaua wanajeshi 20

Image caption Wapiganaji wa Taleban

Wanajeshi 20 wa serikali ya Afghanistan wameuawa mashariki mwa taifa hilo katika kile kinachoonekana kuwa kisa kibaya zaidi dhidi ya vikosi vya usalama katika kipindi cha mwaka mmoja.

Shambulizi hilo lilitokea wakati wa usiku katika mkoa wa Kunar wakati watu waliojihami kwa bunduki walipokishambulia kizuizi kimoja cha barabarani katika eneo hilo la milima linalopakana na taifa la Pakistan.

Wapiganaji wa Taleban wameiambia BBC kwamba waliwatekanyara wanajeshi wengine na kwamba wao ndio waliohusika na shambulizi hilo.

Kulingana na mwandishi wa BBC watu waliojihami kwa bunduki walikivamia kizuizi kimoja cha barabara katika shambulizi ambalo waziri wa Ulinzi amedai lilihusisha mamia ya wapiganaji wa kigeni pamoja na wale wa Afghanistan.

Wanajeshi 20 waliuawa katika ufyatulianaji huo wa risasi katika eneo hilo la mashambani la mashariki mwa Afghanistan huku mmoja ya wavamizi hao pia akipoteza maisha yake.

Mapigano zaidi yaliendelea hadi masaa ya asubuhi huku wapiganaji hao wakifyatua risasi zao kutoka maeneo ya juu ya milima.

Rais Hamid Karzai ameshtumu mauaji hayo na kuahirisha ziara yake nchini Sri lanka.

KIongozi huyo ametoa wito kwa serikali jirani ya Pakistan kuharibu kile alichokitaja kama makundi ya kigaidi ambayo amesema hutekeleza mashambulizi ya mipakani.

Msemaji wa kundi la Afghanistan ameiandikia barua BBC akikiri kwamba kundi hilo ndilo lililohusika na shambulizi na kuongezea kuwa wanajeshi saba wa Afghanistan wametekwanyara na kundi hilo.