Kikosi cha usalama chafutwa Ukraine

Waandamanaji wa Ukraine Haki miliki ya picha n
Image caption Baadhi ya waandamanaji wamelaumiwa kwa kuwa na silaha huko Ukraine

kaimu Waziri wa usalama wa ndani wa Ukraine amesema kikosi maalum cha usalama kilicholaumiwa kwa kuwaua waandamanaji kimefutwa. Arsena Avakov amesema taarifa zaidi kuhusu masuala ya usalama nchini humo zitaendelea kutolewa kwa umma.

Wakati huo huo jamii ya kimataifa imeendelea kugawanyika kufuatia kuondolewa madarakani kwa Rais Viktor Yanukovych. Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov ameomba mataifa kulaani kampeini ya uzalendo inayoshinikizwa na upande wa Magharibi mwa Ukraine.

Bw Lavrov hasa amekosoa vikali sheria ya kupiga marufuku utumizi wa lugha ya Kirusi pamoja na tisho la kuwafutia uraia raia wanaozungumuza lugha hiyo ndani ya Ukraine.Urusi imetaja kuondolewa kwa Yanukovych kama mapinduzi ya nguvu na imeelezea wasi wasi kuhusu kampeini inayoendeshwa na mirengo ya kuzalendo inayopinga vikali Urusi.

Ndani ya Ukraine maeneo yanayozungumza Kirusi hasa Mashariki na Kusini mwa nchi yamepinga kuondolewa kwa Rais Vicktor Yanukovych. Katika eneo la Crimea wakaazi na utawala wa eneo hilo umepandisha bendera ya Urusi na kuondoa ile ya Ukraine.

Urusi imesema haitaingilia masuala ya ndani ya Ukraine. Kwa upande mwingine Marekani na nchi washirika wake Barani Ulaya zinaunga mkono upinzani na kutambua mamlaka ya sasa.