Uzembe wa jeshi waudhi wakaazi Nigeria

Haki miliki ya picha yobe govt
Image caption Ibrahim Geidam gavana wa jimbo la Yobe,Nigeria

Wakaazi wa mji mmoja kaskazini mashariki mwa Nigeria wameonyesha hasira dhidi ya majeshi ya usalama kwa kuondoa vituo vya ukaguzi kabla ya shambulio la wapiganaji wa Kiislam katika shule shule moja katika eneo hilo.

Vijana wapatao 29 waliuawa katika shambulio hilo, ambapo kikundi cha Boko Haram kimeshtumiwa kuishambulia shulehiyo iliyopo jimbo la Yobe.

Wakaazi wanasema askari waliokuwa wakilinda katika kituo jirani cha ukaguzi, waliondolewa katika hali isiyotarajiwa kabla ya shambulio hilo.

Kituo kingine nje ya mji wa Buni Yadi pia walinzi wake waliondolewa wiki moja iliyopita.

Wanamgambo hao wa Kiislam waliishambulia shule hiyo usiku wa Jumatatu wiki hii.

Gavana wa jimbo la Yobe, Ibrahim Gaidam pia ameyashutumu majeshi ya usalama kwa ugoigoi mkubwa ulionyeshwa katika kukabiliana na tukio hilo, akisema saa tano zilipita bila ya askari wa usalama kuwasili katika eneo la tukio ili kuzima mauaji hayo.