Shambulizi lawaua 12 Mogadishu

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mogadishu imeshuhudia mashambulizi ya mara kwa mara hivi karibuni

Mshambuliaji wa kujitoa muhanga amejilipua ndani ya gari na kuwauwa watu 12 na kujeruhi wengine wanane mjini Mogadishu Somalia.

Mlipuko huo umetokea nje ya makao makuu ya maafisa wa usalama .

Mwandishi wa BBC anasema kuwa waliofariki ni maafisa usalama na wengine raia wa kawaida waliokuwa katika mkahawa karibu na hapo.

Kumekuwa na ongezeko la mashambulizi huku vikosi vya nchi hiyo vikipambana na wanamgambo wa al shaabab.

Kundi la wanamgambo la Al Shabaab limekiri kufanya shambulizi hilo ambalo limetokea chini ya wiki mbili baada ya kundi hilo kushambulia ikulu ya Rais mjini Mogadishu

Msemaji wa kijeshi wa kundi hilo amenukuliwa na shirika la habari la Reuters akisema kuwa huu ndio mwanzo tu wa kundi hilo kushambulia Mogadishu na kwamba operesheni yao itaendelea.

Alisema kuwa shambulio hilo lililenga maafisa wa usalama waliokuwa wameketi katika mkahawa mmoja na kuwaua watu 11 huku 15 wakijeruhiwa.

Polisi walisema kuwa takriban watu 10 walifariki katika mkahawa huo ambao unapendwa sana na maafisa wa usalama.

Ingawa kundi la Al Shabaab liliondolewa kutoka mjini Mogadishu na miji mingine, lingali linadhibiti sehemu kubwa za nchi hiyo.

Pia limekuwa likifanya mashambuzli makali dhidi ya serikali na kutatiza juhudi zake za kutaka kudhibiti baadhi ya sehemu za nchi hiyo