Mswada wa kuwabagua mashoga wakatiliwa.

Haki miliki ya picha AP
Image caption waharakati wa kupigania haki za mashoga

Gavana wa jimbo la Arizona nchini Marekani ameukataa mswada ambao ungesababisha kubaguliwa kwa watu wa jinsia moja.

Ijapokuwa sheria hiyo ilipitishwa na bunge la sineti la jimbo hilo, ulihitaji sahihi ya gavana huyo lakini baada ya shinikizo kutoka kwa wafanyibiashara na wanasiasa kutoka pande zote mbili akalazimika kuufutilia mbali.

Mswada huo ulitarajiwa kulinda uhuru wa kidini,lakini pia ungewapatia haki ya kisheria wale wanaowabagua wenzao.

Wenye mswada huo wanasema kwamba watu wanapaswa kuwa na uhuru wa kutowauzia kitu ama hata kuwahudumia watu wa jinsia hiyo iwapo ni kinyume na dini.

Wanasema kuwa sheria hiyo ingewakubalia wenye maduka kuweka alama ambazo zinapinga kuwahudumia mashoga.

Mswada huo ulipitishwa na bunge la sineti la Jimbo hilo lakini ukahitaji sahihi ya gavana Jan Brewer ili iwe sheria.

kupitishwa kwa mswada huo na bunge la sineti kulizua pingamizi kutoka kwa makundi ya haki za mashoga ,wafanyibiashara na wanasiasa.

Gavana huyo alishinikizwa kuupinga mswada huo na kampuni ya Apple ambayo inajenga kiwanda kipya katika jimbo hilo,shirika la ndege la American Airline ambalo linaandaa mchuano ya Superbowl pamoja na masineta watatu wa chama cha Republican ambao walikuwa wameunga mkono mswada huo lakini wakabadili msimamo wao .