Bunge la Crimea laitisha kura ya maoni

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wafuasi Crimea wanaoegemea upande wa Urusi

Bunge huko Simferopol katika eneo la Crimea limetoa wito wa kufanyika kura ya maoni kuhusu kujitenga kikamilifu, wakati hofu ya mzozo wa kujihami ikiongezeka.

Watu waliojihami wanaounga mkono kuegemea kwa Urusi wanalidhibiti bunge na mijengo ya serikali huko Simferopol, na makundi ya watu nje ya maeneo hayo wanashinikiza kampeni yao ya kulidhibiti kisiasa kikamilifu eneo la Crimea.

Mapema hii leo, aliyekuwa Rais wa Ukraine Viktor Yanukoovich, anasemekana kuonekana nchini Urusi baada ya kutoweka kwa siku kadhaa.

Hii ni kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Urusi ambavyo vimenukuu taarifa kutoka kwake.

Lakini bado hakuna taarifa kamili kuhusu aliko hasa.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Viktor Yanukovych anasema angali Rais wa Ukraine

Yanukovych aomba kulindwa

Katika taarifa yake alisema kuwa bado yeye ni Rais wa Ukraine ingawa anaitaka serikali ya Urusi kuhakikisha usalama wake.

Taarifa hiyo, kutoka kwa Viktor Yanukovych ilitolewa na shirika rasmi la habari la Urusi na kusomwa kwenye televisheni nchini humo

Katika taarifa hiyo amesema kuwa yungali Rais wa Ukraine na anaamini kwamba vikao vya wabunge vinavyoendelea katika bunge la Ukraine sio halali.

Alisema kuwa ameitaka Urusi kumlinda kutoka kwa watu wenye siasa kali ambao walitwa mamlaka nchini Ukraine.

Aliongeza kuwa watu wa Kusini na Mashariki ya Ukraine na katika eneo la Crimea hawatakubali hali mbaya ya kisiasa ambapo mawaziri wa serikali wanaidhinishwa na makundi ya watu na kuonya dhidi ya kutokea vita vya wenyewe kwa wenyewe katika siku zijazo.

Alikanusha madai kuwa aliamuru wanajeshi kuingilia mzozo wa kisiasa nchini humo na kuwa hatafanya hivyo kamwe ila ataendelea kutafuta suluhu.