Uhalifu wa hisa kutokomezwa Ulaya

Image caption Magenge hayo huwahadaa watu kuekeza katika hisa bandia

Polisi wa Ulaya wakishirikiana na wale wa Marekani, wamefanya msako mkubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa dhidi ya magenge ya wahalifu.

Msako huo, ulilenga makundi ambayo huwahadaa watu kuekeza katika hisa zisizokuwa na thamani, wakiwaahidi mapato mazuri.

Msako huo, ulifanyika nchini Uingereza, Serbia, Uhispania na Marekani.

Zaidi ya watu miamoja wamekamatwa wengi wao nchini Uhispania. Magenge haya yanaishi maisha ya kifahari yakimiliki magari na nyumba za kifahari.

Pesa na bidhaa za kifahari pamoja na magari ya kifahari yalinaswa katika msako huo.

Inakisiwa kuwa watu 850 walihadaiwa na magenge hayo nchini Uingereza lakini huenda idadi hiyo ni kubwa zaidi na kupoteza mamilioni ya dola wakitarajia kufaidika katika masoko ya hisa.

Majasusi wanasema kuwa lengo la uchunguzi huo uliofanyika kwa miaka miwili, ni kuangamiza uhalifu wa aina hiyo barani Ulaya.

Wanaamini kuwa msako huu ni mkubwa zaidi kuwahi kufanyika dhidi ya wahalifu hao. Msako huo ulijulikana kama 'Operation Rico' na uliongozwa na polisi wa Uingereza.