Wapiganaji waua watu 29 Borno

Haki miliki ya picha Reuters

Kundi la wapiganaji waisilamu limewaua takriban watu 29 katika mji mmoja kaskazini mashariki mwa Nigeria, jimbo la Borno.

Vikosi vya usalama vya kiserikali vilitoroka pale ambapo kundi hilo lilishambulia mji wa Mafa Jumapili usiku.

Mashambulizi hayo yanaifikisha idadi ya mauaji ya watu yaliyotekelezwa katika jimbo la Borno kuwa takriban 150 tangu Ijumaa tokea kuchipuka kwa mashambulizi hayo. Hii ni kulingana na taarifa zilizotolewa.

Kundi la wapiganaji la Kislamu la Boko Haram limekuwa likihangaisha watu nchini Nigeria kwa muda sasa.

Mwezi Mei mwaka jana, Rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan, alitangaza hali ya hatari Borno na majimbo mengine mawili na kuipa jeshi mamlaka zaidi ili kukabiliana na ghasia hizo ambazo zimedumu kwa miaka minne sasa.

Ila, kundi la Boko Haram limekuwa likitekeleza mashambulizi ya kuvizia, kwani wamekuwa wakifanya mashambulizi mapya katika maeneo tofauti kila siku, anasema mwandishi wa BBC, Will Ross, ambaye yuko Nigeria.

Maelfu ya watu wamepoteza maisha yao na mamia wengine kutoroka makwao kutokana na makali ya mashambulizi hayo.

'Mashambulizi yanayotekelezwa hewani'

Bw. Zannah ambaye ni seneta kutoka jimbo la Borno, aliiambia BBC dira ya dunia kuwa kundi la Boko Haram lilikuwa limetoa onyo la kushambulia mji wa Mafa.

Shule zilifungwa, na wenyeji wengi kutoroka makwao, na kuelekea jiji la Maiduguri ambalo liko takriban umbali wa kilomita 45 kutoka Mafa.

Ingawa idadi zaidi ya wanajeshi walitumwa Mafa, bado hawakutosha, na pia hawakuwa na vifaa vya kutosha vya kukabiliana na mashambulizi hayo.

Hapo awali siku ya Jumamosi, mabomu mawili yaliyolipuliwa Maiduguri, yaliwaua watu 50-jiji ambalo Boko Haram limekuwa likilenga kwa muda mrefu sasa.

Seneta wa jimbo la Borno, Ali Ndume, aliambia BBC kuwa takriban watu 20; wengi wao wakiwa wakongwe waliuliwa pale ambapo jeshi la nchi hiyo lilifanya mashambulizi ya hewani katika kijiji cha Daglun Ijumaa usiku. Ingawa wizara ya Ulinzi ilikanusha madai hayo.

"Ripoti hizo ni njama tu zinazonuia kudunisha na kuathri kujitolea kwetu kupigana vita dhidi ya ugaidi,” msemaji wa wizara hiyo, Chris Olukoladehe, aliambia shirika la habari la AFP.

Alisema kuwa vikosi vya kiserikali viliweza kuwaua waasi kadhaa wa kundi la Boko Haram katika operesheni iliyotekelezwa Jumapili usiku.

Boko Haram ambao wanashukiwa kuyafanya mashambulizi katika eneo la Maiduguri wametiwa mbaroni.