Magari ya umma yavuruga shughuli Nairobi

Image caption Mgomo wa wahudumu wa magari nchini Kenya

Huduma za usafiri jijini Nairobi zimekwama kufuatia hatua za wenye magari kugoma hii leo wakilalamikia nyongeza ya ada ya kuegesha magari jijini humo.

Maelfu ya wafanyakazi wamelazimika kutembea kwa miguu na wasafiri wa kutoka jijini kwenda maeneo ya mashambani nao kulazimika kuahirisha safari zao.

Mwenyekiti wa wenye matatu katika eneo la Mlima Kenya, Bwana Michael Kariuki, ambaye aliongea na BBC akiwa nje ya lango la kuingia kwenye afisi ya Gavana wa Kaunti ya Nairobi, alisema mzozo uliopo ni mdogo na waweza kusuluhishwa haraka.

"Juzi tulikuwa na Gavana Evans Kidero na tukakubaliana kiasi tunachopaswa kulipa lakini jana tulipofika wafanyakazi wa kaunti wakakataa kiasi tulichokuwa nacho," Bwana Kariuki alisema.

Image caption Wahudumu wa magari ya umma wakigoma Nairobi

Jiji la Nairobi ni mojawapo wa kaunti ambazo zimebuniwa chini ya Katiba iliyopitishwa na wapiga kura na kuidhinishwa mwaka 2010 katika hatua ya kuimarisha huduma kwa wananchi.

Kaunti hizo mpya hata hivyo zimejikuta njia panda baada ya kupata madaraka bila fedha za kuandamana nayo; ambapo zimelazimika kuongeza kodi kama njia mojawapo ya kujiimarisha kiuchumi.

Mkuu wa polisi nchini Kenya, David Kimaiya aliagiza idara ya trafiki nchini Kenya kunasa magari yote yaliyofunga barabara za mji.

Image caption Maafisa wa polisi wakingoa nambari za usajili za magari ya umma yaliyogoma mjini Nairobi