Obama amualika Waziri Mkuu wa Ukraine

Haki miliki ya picha UNIAN
Image caption Arseniy Yatsenyuk

Rais wa Marekani Barrack Obama, amemualika waziri mkuu wa Ukraine, Arseniy Yatsenyuk, mjini Washington kwa mashauriano kuhusiana na mzozo unaokumba taifa lake.

Ikulu ya White House, imesema kuwa mkutano huo utakaofanyika siku ya Jumatano, utaangazia, mbinu za kutafuta suluhisho la amani, kuhusiana na operesheni za kijeshi zinazoendesha na jeshi la Urussi katika eneo la Crimea.

Waandishi wa habari wanasema kuwa mualiko huo ni ni ishara thabiti kuwa Marekani inaunga mkono utawala wa mpito wa Kiev.

Wakati huo huo, jamii ya kimataifa inaendelea kuishinikiza utawala wa Moscow, kuondoa wanajeshi wake katika eneo la Crimea.

Chansella wa Ujerumani, Angela Merkel, amemueleza rais wa Urussi, Vladimir Putin, kutilia maanani kuwa kura ya maoni kuhusu ikiwa eneo hilo la Crimea, litajiunga na Urussi inakiuka sheria na ni haramu.

Khodorkovsky apinga utawala wa Moscow

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais Obama

Huku hayo yakijiri, mfungwa wa zamani na mfanya biashara maarufu wa secta ya mafuta na mkoasoaji mkubwa wa rais Putin, Mikhail Khodorkovsky, anehutubia mkutano mkubwa wa hadhara katika mji mkuu wa Ukraine Kiev.

Amewaambia maelfu ya watu waliofurika katika medani ya Uhuru kuwa serikali ya Urussi inawahadaa raia wake kwa kuwahusisha waandamanaji mjini Kiew na watu wanaopinga utawala wake na raia wake.

Mikutano kama hiyo imefanyika katika sehemu kadhaa za nchi hiyo.

Nyingi zikiwa za amani lakini mjini Sevastopol, katika eneo la Crimea, raia wa Ukraine wanaozungumza lugha ya Kirussi waliwapiga watu wanaounga mkono serikali ya Ukraine.

Televisheni zilizo na makao yao mjini Kiev zimezuiliwa kurusha matangazo katika eneo hilo la Crimea.