Maandamano kadha yafanywa Ukraine

Wavuvi Sevastopol, Crimea Haki miliki ya picha AFP

Maelfu ya Watu wa Ukraine wamekusanyika katika medani ya uhuru mjini Kiev kutoa wito wa amani na umoja, wakati Urusi inazidi kujizatiti Crimea.

Kati ya wale waliohutubia ni tajiri wa mafuta wa zamani wa Urusi, Mikhail Khodorkovsky, ambaye mara nyingi anailaumu serikali ya Urusi.

Kulikuwa na maandamano kutwa katika miji kadha ya Ukraine.

Mengi yalipita salama lakini katika mji wa Sevastopol wa Crimea, watu wenye asili ya Urusi walitumia bakora kuwapiga waandamanaji wanaoipendelea Ukraine.

Na televisheni zenye makao yake mjini Kiev, zimekatazwa kuripoti kutoka ras ya Crimea.

Na Rais Vladimir Putin wa Urusi amesema hatua zilizochukuliwa na bunge la jimbo la Crimea kutaka kujiunga na Urusi, zinalingana na sheria za kimataifa.

Alisema hayo kwenye mazungumzo ya simu na kiongozi wa Ujerumani, Angela Merkel na waziri mkuu wa Uingereza, David Cameron.

Taarifa ya serikali ya Urusi piya ilisema kwamba viongozi hao walikubaliana kuwa mvutano unafaa kupunguzwa.

Wakati huohuo ikulu ya Marekani imethibitisha kuwa waziri mkuu wa Ukraine, Arseny Yatseniuk, atazuru Washington juma hili kwa mazungumzo kuhusu msukosuko wa Ukraine.

Waziri wa mashauri ya nchi za nje wa Uingereza, William Hague, alisema baada ya muda itabainika kuwa Urusi imefanya makosa makubwa kuivamia Crimea.

Alisema siku za mbele mataifa ya Ulaya yatanunua gesi na mafuta kutoka nchi nyengine badala ya Urusi