Michael Schumacher 'aonyesha dalili nzuri'

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mashabiki wa Schumacher wakimtakia kila la heri

Bingwa wa zamani wa mashindano ya langalanga ya Fomula 1 Michael Schumacher, amekuwa akionyesha dalili nzuri baada ya madaktari kuanza kumtoa katika hali yake mahututi.

Familia yake imesema kuwa ingali ina matumaini kwamba Michael ataweza kuamuka.

Madaktari nchini Ufaransa wamekuwa wakifanya juhudi za kumuamusha Michael ambaye ni bingwa mara saba katoka katika hali yake ya kupoteza fahamu.

Schumacher mwenye umri wa miaka 45 kutoka Ujerumani, alipata majeraha mabaya ya kichwa alipokuwa anashiriki mchezo wa kuteleza kwa barafu mwezi Disemba 29 katika maeneo ya Alps Ufaransa.

Madaktari walimuweka Schumacher katika hali ya kupoteza fahamu ili kuzuia uvimbe katika ubongo wake.

Familia ya Schumacher imezungumza na kusifu jitihada za madaktari wa Ufaransa na pia wamesema kuwa hiki ni kipindi kigumu kwao na kuwa hawana budi ila kuwa na subira.

Wachunguzi wanasema kuwa Schumacher hakuwa anaenda kwa kasi kubwa wakati wa ajali hiyo ingawa alianguka alipokuwa akiteleza.

Schumacher alistaafu kutoka katika mashindano ya langa langa mwaka 2012 baada ya kushiriki mwa miaka 19.

Alishinda mataji mawili akiwa na kampuni ya Benetton mwaka 1994 na 1995,kabla ya kuhamia kampuni ya Ferrari mwaka 1996 na kuendelea kushinda mataji mengine matano kuanzia mwaka 2000.