Bensouda kukata rufaa kesi ya Katanga

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Fatou Bensouda

Mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya Kimataifa ya uhalifu ICC, Fatou Bensouda amesema huenda akakata rufaa hukumu iliyotolewa kwa mbabe wa zamani wa kivita nchini Congo Germain Katanga.

Katanga alipatikana na hatia nne za uhalifu wa kivita na hatia moja ya uhalifu dhidi ya binadamu, lakini akaondolea makosa kuhusu ubakaji.

Wapiganaji wake walishutumiwa kuwabaka wanawake na kuwateka huku wakiwatumia kama watumwa wa ngono.

Makundi ya wanawake nchini Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo yameelezea hasira na masikitiko yao kutokana na hatua ya mahakama hiyo ya ICC ya kumuondolea Bwana Gatanga makosa hayo.

Wakati wa ziara yake katika mji mkuu wa DRC, Kinshasa, Bensouda alisema kuwa huenda akakata rufaa dhidi ya uamuzi huo wa mahakama.

''Majaji hawakumuhumu kuhusiana na mashtaka ya unyanyazaji wa kimapenzi, mashtaka ambayo tulikuwa tumemshtaki nayo, pamoja na ile ya kuwasajili watoto jeshini'' Alisema Bensouda.

Bensouda, amesema kuwa wanachunguza hukumu hiyo kwa undani na kuchunguza ikiwa kuna dosari kadhaa za kisheria ambazo wanaweza kutumia kukata rufaa.

''Majaji kwa hekima zao walihisi kuwa bwana Katanga hakuhusika moja kwa moja na mashtaka hayo. Nadhani waadhiriwa wanafurahia kuwa ofisi yake inafuatilia suala hili, ili kuhakikisha kuwa mashtaka mazito kama hayo yanachunguzwa.'' Aliongeza Bensouda.

Kuhusiana na kesi inayomkabili rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, makamu wake William Ruto na mwandishi wa habari Joshua arap Sang, Bensouda alisema kuwa ''Nimeonyesha wazi kuambatana na ombi niliowasilisha mbele ya mahakama, kuhusiana na changa moto tunazopata, baada ya mashahidi wakuu kujiondoa kwa sababu kadhaa''.

Bensouda amesema kuwa itakuwa vigumu sana kwa ofisi yake kuendelea na kesi hizo kama ilvyopangwa baada ya mashahidi wakuu kujiondoa.

''Nimewafahamisha majaji kuwa tulikuwa na mashahidi kadhaa wakuu ambao walikuwa tayari kutoa ushahidi kuhusiana na matukio muhimu nchini Kenya, lakini wameomba kujiondoa kutoka kwa kesi hiyo.

Na kama unavyofahamu mashtaka haya pia ni mazito, na kabla ya kwenda mahakamani mtu anapaswa kuwa na uhakika wa kuwa na ushahidi ambao utakidhi mahitaji muhimu ili kuhakisha kuwa washukiwa wanahumiwa.'' Alisema Bensouda.