Marekani yasaidia juhudi za Malaysia

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Juhudi zimeelekezwa sasa katika Bahari Hindi

Marekani imetuma watalaamu katika bahari Hindi kujiunga na juhudi za kuisaka ndege ya Malaysia iliyotoweka Jumamosi wiki jana.

Maafisa ambao hawakutaka kutajwa wanasema kuwa ndege hiyo ilituma data ya Satelite kwa zaidi ya saa tano baada ya kutoweka.

Hata hivyo wachunguzi walisema hapajakuwa na tathmini ya kina kuhusu data hiyo ya Satelite kubaini ukweli.

Vyombo vya habari vya serikali ya China vinadokeza kuwa wataalam wanasema huenda ndege hio ilianguka katika ziwa la kusini mwa Nchi hiyo .

Afisa mkuu wa mauzo wa shirika hilo la ndege Hugh Dunleavy amepuuzilia mbali ripoti hizo.

Serikali imesema kuwa msako wa ndege hiyo utaendelea hadi eneo la Magharibi katika bahari Hindi.

Waziri wa usafiri wa Malaysia, Hishammuddin Hussein, amekataa kuzungumzia ripoti za Marekani kuwa Ndege hiyo iliendelea kupaa kwa saa kadhaa kabla ya kutoweka.

Mkuu wa Halmashauri ya usafiri wa ndege nchini Malaysia, Azharuddin Abdul Rahman, amesema kuwa Malaysia inashirikiana na Marekani kubaini ikiwa kuna taarifa zozote za Satelite ambazo zinaweza kusema iliko ndege hiyo iliyotoweka ikiwa imebeba watu 239.