Je ni sawa vyombo vya dola kuharamisha Zinaa?

Image caption Ndoa nyingi zimekuwa zikivunjika kutokana na Zinaa

Zinaa imeharamishwa na dini nyingi karibu zote kama sijakosea. Lakini je umewahi kutafakari kama Zinaa iharamishwe na vyombo vya dola?

Mwishoni mwa wiki nchini Kenya mwanamume mmoja alimpata mkewe akila uroda na mwanamume (mpango wake wa kando) katika chumba kimoja cha hoteli mjini Nairobi.

Hasira na ghadhabu zilimsababisha mwanamume huyo wapeleka mkewe pamoja na mwanamume aliyemkamata naye katika kituo cha polisi kuwashitaki kwa kosa hilo.

Taarifa hii iliwaacha wengi wakipiga gumzo katika mitandao ya kijamii nchini Kenya.

Baadhi wakisema kuwa Zinaa ni mbaya sio katika ndoa tu bali hata kama hujaolewa, basi ikiwa imefikia kiwango cha kuhusisha polisi basi iharamishwe kisheria na ikiwa mtu atapatikana akishiriki zinaa ashitakiwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Je vyombo vya dola vina jukumu lolote katika kurekebisha maadili ya watu?

Mnamo mwaka 2007, Uganda ilifutilia mbali sheria yake dhidi ya Zinaa baada ya wanaharakati kusema kuwa iliwaonea zaidi wanawake kuliko wanaume. Mwanamke ambaye angpetikana akizini angefungwa jela.

Nchini Kenya katika siku za hivi karibuni, visa vya wanandoa kukamatwa wakishiriki Zinaa vimeongezeka, sio mapasta, sio wahubiri, visa hivi vimekuwa vingi tu.

Mhubiri mmoja aliyepatikana akishiriki Zinaa na mke wa mtu mjini Kisimu Magharibi mwa Kenya, alitembezwa uchi pamoja na mwanamke na wananchi waliochukua sheria mikononi mwao na kulazimisha polisi kuingilia kati.

Kwani hili swala ni la kuwahusisha polisi?

Je nini maoni yako kuhusu hoja hii:Zinaa iharamishwe na vyombo vya dola au la? Tuma maoni yako kupitia ukurasa wetu wa Facebook https://www.facebook.com/pages/BBC-Swahili/160894643929209?ref=hl