Watuhumiwa kufikishwa mahakamani Kenya

Image caption Mombasa imesemekana kuwa kitovu cha itikadi kali za kidini kwa vijana waisilamu

Washukiwa wawili waliopatikana na mabomu mawili makubwa katika mji wa Mombasa Pwani ya Kenya, wanatarajiwa kufikishwa mahakamani baadaye leo.

Wawili hao walizuiliwa na polisi mjini Mombasa baada ya kupatikana na mabomu hayo ndani ya gari lao. Inaarifiwa walinuia kutekeleza shambulizi kubwa mjini Mombasa ingawa walikamatwa na polisi wa kupambana na ugaidi.

Maafisa wanasema kuwa mabomu hayo yalitarajiwa kuteguliwia huko Mombasa.

''Wanaume hao walikamatwa na mabomu makubwa yanayodhaniwa kuwa yangetumiwa kushambulia bandari ya Mombasa'', alisema afisa wa ngazi ya juu wa polisi.

Wanakabiliwa na tuhuma za ugaidi na kumiliki silaha kinyume na sheria.

Kundi la wanamgambo wa Alshaabab la Somali limedai kutekeleza mashambulio kadhaa nchini Kenya.

Baada ya shambulio la Westgate jijini Nairobi lililowauwa takriban watu 67, kundi hilo linasema lilipanga mashambulio zaidi .

Eneo la pwani ya Kenya ambalo ni maarufu kwa utalii limekuwa likilengwa kwa mashambulizi na pia limegeuka na kuwa kitovu cha vijana kujiingiza katika itikadi kali za dini.

Kundi la Al Shabaab limekuwa likidai vikosi vya Kenya viondoke kutoka Somalia ambako vimekua vikipigana na waasi wa kiislam.

''Tunashuku kuwa ni watu hawa ni wa kundi la Al Shabaab hasa kutokana na asili yao", alisema mkuu wa polisi eneo la Mombasa Robert Kitur, na kuongeza kuwa mmoja wao alikuwa msomali na wapili alikuwa mkenya mwenye asili ya Somali.

Kenya ambayo ni nchi jirani na Somalia ina idadi kubwa ya raia wenye asili ya kisomali

Taarifa ya kukamatwa kwa wili hao zimegonga vyombo vya habari katika nchi ambayo imekuwa ikikumbwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya maguruneti na mabomu.