Maafisa wadhibiti ulinzi Kenya

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Maafisa polisi wakishika doria Kenya

Maafisa wa usalama nchini Kenya wamedhibiti ulinzi baada ya kunasa silaha nzito kutoka kwa watu wanaoshukiwa kuwa magaidi mjini Mombasa Pwani ya Kenya

Siku ya Jumatatu maafisa wa polisi mjini humo, walipata mabomu mawili makubwa ndani ya gari liliokuwa limeegeshwa katika kituo cha polisi.

Maafisa hao pamoja na wataalamu wa kutegua mabomu kutoka nchini Marekani walisema kuwa mabomu hayo yalikuwa na uwezo wa kusababisha uharibifu mkubwa sana na hata kuangusha jengo la ghorofa 14.

Siku ya Jumatatu watu wawili walioshukiwa kuwa wanachama wa kundi la wanamgambo la Al Shabaab, walikamatwa wakiwa na mabomu hayo katika mtaa wa Changamwe mjini Mombasa.

Hali ya usalama nchini Kenya hususan mjini Mombassa ambako vijana wa kiisilamu wanatuhumiwa kwa kujiingiza katika itikadi kali za kiisilamu umekuwa ukisuasua.

Mshukiwa wa tatu alikamatwa Jumanne akiwa na vilipuzi vingine. Kundi la kigaidi limekuwa likisema kuwa litaendelea kushambulia Kenya hadi itakapoondoa majeshi yake nchini Somalia.

Mwaka jana kundi hilo lilifanya shambulizi kubwa zaidi la kigaidi kuwahi kushuhudiwa katika miaka ya hivi karibuni na kuangusha jumba la kifahari la Westgate pamoja na kuwaua zaidi ya watu sitini na mamia ya wengine wakijeruhiwa vibaya.

Kenya ni miongoni mwa nchi za Afrika ambazo zina wanajeshi wake nchini Somalia wanaopambana na wanamgambo wa Al Shabaab. Hapo jana Uganda pia ilitoa tahadhari kuhusu njama ya Al Shabaab kushambulia nchi hiyo kwa kutumia malori ya mafuta kama mabomu.