Mahakama yaruhusu mkenya kufikishwa ICC

Image caption Walter Baraza anatuhumiwa kwa kosa la kjuwahonga mashahidi katika kesi dhidi ya William Ruto ICC

Mahakama kuu nchini Kenya imepinga agizo la kutokamatwa kwa mwandishi Walter Baraza baada ya wakili wake Kibe Mungai kushindwa kufika mahakamani ili kusikilizwa kwa kesi hiyo.

Hatua hiyo inamaanisha kwamba waziri wa usalama nchini Kenya Joseph Ole Lenku anaweza kuomba agizo la kukamatwa kwa mwandishi huyo kabla ya kuwasilishwa katika mahakama ya ICC anakotakikana kwa kosa la kuwahonga mashahidi.

Walter Baraza anatakikana na mahakama hiyo kwa madai ya kuingilia ushahidi katika kesi inayomkabili makamu wa rais wa kenya William Ruto.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais Kenyatta na makamu wake wamefikishwa ICC kwa kosa la kuhusika na ghasia za kikabila 2007/08

Uamuzi wa Jaji wa Mahakama Kuu Richard Mwongo ni pigo kubwa kwa Mwandishi wa habari Walter Barasa, ambaye alikuwa aking'ang'ana kuhakikisha kuwa hakamatwi na kusafirishwa hadi Hague kushtakiwa kwa kosa la kuwahonga mashahidi waliokuwa wameorodheshwa na kiongozi wa Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu.

Mwaka uliopita Kiongozi wa mashtaka katika The Hague, Fatou Bensouda, alitoa ombi ambalo lilikubaliwa na kuwasilishwa nchini Kenya ambapo ilitakiwa Waziri wa Maswala ya Usalama Joseph Ole Lenku aagize Walter akamatwe na kufikishwa ICC.

Katika agizo hilo ilidaiwa kuwa Bwana Barasa alitumia pesa kuwahonga mashahidi waliotarajiwa kutoa ushahidi dhidi ya Naibu Rais wa Kenya, William Ruto na mtangazaji Joshua arap Sang.

Wakenya hao wawili wameshtakiwa kuwa walichangia pakubwa katika kuchochea ghasia za baada ya Uchaguzi wa mwaka 2007/08 ambapo zaidi ya watu 1,300 waliuawa katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe baada ya upande wa upinzani kupinga matokeo ya uchaguzi.