4 hatiani kwa kumbaka mpigapicha India

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wanawake hawa wanakerwa na kiwnago cha juu cha dhuluma dhidi ya wanawake

Mahakama moja katika mji wa Mumbai nchini india imewapata na hatia watu wanne kwa kosa la kumbaka mpiga picha mmoja mwaka jana.

Wanne hawa wamepatikana na hatia ya mashtaka tano yakiwemo ya kumbaka mwanamke huyo kwa pamoja, kuhusika kwa ngono isiyo ya kawaida pamoja na kuharibu ushahidi.

Hukumu dhidi yao inatarajiwa kutolewa siku ya ijumaa.

Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 22 alikuwa anajifunza kazi ya uandishi katika kampuni ya jarida la kiingereza lenye makao yake mjini Mumbai.

Alishambuliwa na wanaume watano alipokuwa akiendesha shughuli za kikazi, katika kiwanda cha kutengeneza nguo cha Shakti ambacho hakitumiki tena.

Wakati wa kisa hicho mwathiriwa alikuwa na mwenziwe wa kiume ambaye alipokea kipigo.

Kesi dhidi ya mshtakiwa wa tano ambaye anaaminika kuwa alikuwa wa chini ya umri wa miaka 18 wakati wa kitendo hicho inaendelea katika mahakama ya watoto.

Waziri wa mambo ya ndani wa jimbo la Maharashta RR Patil aliyekuwa kortini wakati wa maamuzi hayo alisema kuwa uamuzi huo ulikuwa wa haki na kuwa kama onyo kwa wengine wasifanye jambo kama hilo.

Kesi hii ilizua kwa mara nyingine tena hisia kali nchini India kuhusu dhuluma za kijinsia, jambo ambalo lilijiri baada ya maandamano ya kitaifa mwezi Disemba mwaka wa 2012 baada ya mwanafunzi mmoja mwenye umri wa miaka 23 kubakwa na genge la vijana katika kituo cha mabasi katika mji mkuu wa Delhi.

Msichana huyo alifariki kutokana na majeraha yaliyo sababishwa na kitendo hicho.Kufuatia kisa hicho wanaume wanne wamehukumiwa kifo huku mshitakiwa mwingine mwenye umri wa chini ya miaka 18 akifungwa katika jela ya watoto.