Marekani , Urusi zazozana kuhusu Crimea

Image caption Mabalozi wa Marekani na Urusi wameshambuliana katika Umoja wa mataifa.

Majibizano makali yameshuhudiwa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambapo mataifa mengi yameshutumu

uamuzi wa Urusi kunyakua eneo la Crimea.Majibizano makali pia yaliibuka kati ya balozi wa Marekani na

Urusi katika kikao hicho.

Balozi wa Urusi, Vitaly Churkin, amesema kuwa watu wa Crimea wamefanya uamuzi kuhusu mustakabali wao.

Naye Balozi wa Marekani, Samantha Power amesema kile kinachotajwa na Urusi kuwa kura ya maoni ni kura batili.

Akionyesha kukasirishwa na matamshi ya Power, Bwana Churkin amesema Balozi Power alikuwa amejishushia hadhi kufikia

kiwango cha magazeti ya udaku.

Balozi huyo wa Urusi pia ametishia kuwa huenda Urusi ikakataa kushirikiana na Marekani katika masuala mengine muhimu

ya kimataifa iwapo Marekani itaendelea na msimamo wake kuhusu Ukraine.

Majibizano hayo makali yanaendelea wakati Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon akitarajiwa kwenda Urusi kufanya

mashauriano na Rais Putin kwa lengo la kutafuta suluhu ya kidiplomasia.

Mkuu wa Majeshi nchini Ukraine, Andriy Parubiy, amesema Serikali yake inafanya kila juhudi kuwarejesha nyumbani

wanajeshi wake na familia zao walio eneo la Crimea, kufuatia hatua ya Urusi kunyakua Crimea.