Wafuasi wa upinzani kuhukumiwa Burundi

Image caption Alexis Sinduhije, kiongozi wa chama cha upinzani MSD

Hukumu dhidi ya wafungwa sabini wa kisiasa wakiwemo wafuasi wa chama cha upinzani MSD waliokamatwa mapema mwezi huu kwa shutuma za kuzua vurugu itatolewa hivi leo mjini Bujumbura.

Tayari kiongozi wa mashitaka ametaka wafungwa 48 kati ya hao sabini kupewa hukumu ya kifungo cha maisha jela.

Kesi hii inaendeshwa katika mahakama ya manispaa ya Bujumbura wilaya ya Ngagara ,ambako Jumanne iliyopita mahakama ilisikiliza kesi za washitakiwa 69.

48 walifikishwa mahakamani kwa kosa la kuzua vurugu tarehe nane mwezi huu katika makao makuu ya chama cha upinzani cha MSD.

Mwendesha mashitaka wa manispaa aliwaombea kifungo cha maisha jela. 17 walikamatwa maeneo mbali mbali ya jiji wakiwa wanafanya mazoezi ya mwili. Hao wameombewa kifungo cha miaka 15 kila mmoja.

Washitakiwa watatu waliachiwa kwa kutopatikana na hatia. Pia kuna watoto wawili ambao wako chini ya umri wa miaka 18 haijajulikana hatma yao kwa kuwa kesi yao inaendeshwa faraghani.

Washitakiwa wote hawa watajibu baadae hii leo mashitaka dhidi yao kuhusu uhatarishaji wa usalama wa umma,kushiriki katika harakati za kuhatarisha usalama na kuwashambulia nakuwajeruhi polisi.

Baadhi ya washitakiwa walijaribu awali kujitetea kuwa hawahusikina na chama chochote cha siasa na kuwa siku hiyo walikuwa wakifanya mazoezi ya mwili kibinafsi .

Umoja wa mataifa na muungano wa Ulaya umeshutumu serikali ya Burundi kwa kukandamiza upinzani.