Jumba la wafu na wafungwa la Nigeria

Image caption Dirisha la gereza lililobanwa kwa vyuma

Polisi wa Nigeria wanasema wamegundua miili kadha iliyooza, mafuvu na viungo vengine vya binaadamu katika jengo lilohamwa katika mji wa Ibadan, kusini magharibi mwa nchi.

Watu kadha wenye utapia mlo wamepatikana karibu na hapo, na vyombo vya habari vya Ibadan vimeripoti kuwa watu kama 15 wamepatikana wakiwa wamefungwa minyororo kwenye uwa wa jengo hilo.

Polisi wamewakamata watu kadha, lakini washukiwa wakubwa bado hawajapatikana.

Maiti hao waligunduliwa baada ya madereva wa pikipiki za boda-boda kuripoti kwa polisi kuwa baadhi ya madereva wenzao walikuwa wametokweka.

Tukio hili limewashangaza watu wengi sana huku miongoni mwa miili iliyopatika ikiwa ya wanaume 18 na wanawake 5.

Watu waliokuwa hai walipatikana vichwa vyao vikiwa vimenyolewa huku wakiwa wamefungwa kwa minyororo.

Mwanamke mmoja alijifungua mtoto Jumamosi katika jumba lenyewe ingawa mtoto wake aliuzwa. Alipoulizwa alivyojipata ndani ya jumba hilo, alishindwa hata kutamka neno na kisha kuzirai.

Takriban watu 9 walipatwa walikuwa wamelala sakafuni wakiwa na utapia mlo na wasiweze hata kuongea.

Nje ya jengo kulikuwa na kaburi lililokuwa wazi ambapo maiti walikuwa wakizikwa.

Inaarifiwa watu mashuhuri hutembelea jengo hilo hasa nyakati za usiku.