Boti ya wakimbizi yazama Ziwa Albert

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wakimbizi mashariki mwa Congo

Miili 25 imepatikana Ziwa Albert baada ya boti iliyokuwa imebeba wakimbizi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuzama.

Wakimbizi hao walikua wakitoroka kutoka kambi ya wakimbizi ya Kyangwali wilayani Hoima magharibi mwa Uganda, wakirejea kwao.

Kwa sasa Jeshi la polisi linaendelea na jitihada za kutafuta miili zaidi. Kamanda wa polisi wa eneo hilo John Ojukuna amesema watu 43 wameokolewa.

Boti iliyozama ilikua imebeba zaidi ya wakimbizi 100.

Wengi wa wakimbizi hao ni wale waliokimbia mapigano mashariki mwa Congo mwaka jana.

Aliyekuwa anaendesha boti hiyo amekamatwa na jeshi la polisi na inadaiwa kuwa alikua mlevi.

Hii sio mara ya kwanza ajali ya boti kuua watu katika Ziwa Albert kutokana na kujaza abiria na mizogo kupita kiasi.

Miaka minne iliyopia boti nyingine ilizama na kusababisha vifo vya watu 70.