Mtoto Cyprian kupokea matibabu Nairobi

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Moses Gift anampakata kakake mdogo Cyprian baada ya kunusurika kifo

Huku hali ya taharuki ikiendelea kutanda mjini Mombasa pwani ya Kenya ambapo magaidi walivamia kanisa siku ya Jumapili na kuwapiga risasi waumini, mmoja wa waathiriwa wa shambulizi hilo amefikishwa Nairobi mwa matibabu maalum.

Shirika la madaktari la AMREF, limemleta Nairobi Mtoto Cyprian Osinya mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu kutoka Mombasa kwa matibabu maalum ya upasuaji wa kichwa baada ya madaktari kugundua kuwa risasi imekwama katika ubongo wake.

Madaktari wanasema kuwa ubongo wa mtoto huyo umefura na kwamba risasi iko upande wa kulia wa ubongo wenyewe. Upasuaji unatarajiwa kufanywa baada ya wiki mbili.

Cyprian amekuwa akihisi uchungu mwingi na hata kukosa usingizi tangu risasi kumuingia kichwani Jumapili.

Mamake aliyekuwa anamkinga kutoka kwa magaidi waliovamia kanisa hilo siku ya Jumapili ,alifariki kanisani humo baada ya kupigwa risasi.

Inaarifiwa risasi aliyomuingia kichwani Cyprian ni risasi iliyomuua mamake kupitia kwa kifua chake na kuishia katika ubongo wa mtoto huyo.

Mamake Cyprian, alikuwa miongoni mwa watu sita waliouawa katika shambulizi hilo, baada ya washukiwa watatu wa ugaidi kulivamia kanisa la Joy in Jesus katika mtaa wa Likoni na kuanza kuwafyatulia waumini risasi kiholela.

Cyprian atafanyiwa upasuaji maalum katika hospitali kuu ya Kenyatta mjini Nairobi ambao utagharamiwa na serikali.