Kenya kutumia ndege kupambana na ujangili

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Uiwindanji haramu wa Ndovu haujaathiri tu Kenya bali Afrika nzima

Kenya inajiandaa kuanzisha mradi wa kutumia ndege zisizokuwa na rubani kuimarisha ulinzi katika mbuga za wanyama, kutokana na kuongezeka kwa visa vya uwindaji haramu.

Mwaka huu pekeee, zaidi ya Vifaru kumi na wanane na Ndovu hamisini na tisa wameuawa huku pembe na meno zao zikiibiwa na kusafirishwa kimagendo hadi nchi za ng'ambo.

Tatizo hili limekithiri sana hali iliyomfanya Rais wa Kenya kutoa wito kwa nchi za afrika mashariki kuimarisha uhusiano wao katika harakati za kutokomeza Ujangili.

Katika kipindi cha miezi mitatu ya kwanza mwaka huu, Kenya imepoteza Vifaru kumi na wanane na Ndovu hamsini na moja kwa wawindaji haramu ukilinganisha na Vifaru 59 na Ndovu 302 waliouawa mwaka uliopita.

Viwango vya uwindaji haramu nchini kenya na katika kanda ya kusini mwa jangwa la sahara vimeongezea katika miaka ya hivi karibuni huku tani kadhaa za pembe za Vifaru na meno ya tembo zikinaswa na maafisa wa ulinzi.

Haki miliki ya picha HONG KONG CUSTOMS
Image caption Biashara haramu ya Pembe za Ndovu imenoga sana katika soko la bara Asia

Naibu mkurugenzi mkuu wa shirika la wanyama pori nchini Kenya Benjamin Kavu anasema kuwa kuzuia uwindaji haramu imekuwa vigumu kwa kuwa hawana vifaa vya kisasa .

Na ili kukabiliana na tatizo hili, la uwindaji haramu, shirika na wanyama pori nchini Kenya KWS pamoja na hifadhi za kibinafsi zimeanzisha mpango wa kutumia ndege zisizokuwa na rubani, ili kuimarisha ulinzi katika mbuga za wanyama.

Tayari majaribio ya ndege hizo yamefanyika katika mbuga ya Ol pajeta na shirika la KWS linatarajiwa kufanya zoezi kama hilo hivi karibu katika mbuga ya Tsavo.

Licha ya kuongezeka kwa idadi ya Vifaru na Ndovu wanaouawa nchini Kenya shirika la KWS limesema kuwa Kenya ingali na idadi ya kutosha kulingana na takwimu za kimataifa na kuwa wameimarisha msako wao dhidi ya wawindaji haramu na wale wanaofadhili shughuli hiyo.

Hata hivyo bei ya juu ya pembe za Vifaru na meno ya tembo imechangia tatizo hili kukithiri.

Akihutubua bunge la afrika mashariki mjini Arusha, rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ameelezea masikitiko yake kuhusiana na kuongezeka la visa vya Tembo na Vifaru kuuawa.

Rais Kenyatta amesema serikali yake itashirikiana na jamii ya kimataifa ili kusitisha biashara ya pembe za faru na Tembo.