Mwathiriwa wa ubakaji kufidiwa Zimbabwe

Image caption Kuavya mimba kumeharamishwa nchini Zimbabwe

Mahakama ya juu zaidi nchini Zimbabwe imeagiza serikali kumlipa fidia mwathiriwa wa ubakaji aliyezuiwa kuavya mimba yake iliyotokana na kitendo cha kubakwa miaka 8 iliyopita.

Mahakama ilikosoa sana polisi na wahudumu wa afya kwa kuchelewa kumsaidia mwanamke huyo kutoa mimba hiyo.

Uavyaji mimba ni haramu Zimbabwe lakini mwanamke anaweza kuruhusiwa kufanya hivyo ikiwa mimba yake imetokana na kitendo cha ubakaji au ikiwa inahatarisha maisha ya mwanamke huyo.

Mtoto wa mwanamke huyo sasa ana umri wa miaka minane na anaenda shule.

Mwandishi wa BBC mjini Harare Brian Hungwe anasema kuwa mahakama ilisema kuwa mafadhaiko aliyoyapa mwanamke huyo kutokana na mimba yalitarajiwa na kwa hivyo madaktari walipaswa kumshauri mwanamke kutumia tembe za kuzuia mimba siku tatu baada ya mwanamke huyo kubakwa mwaka 2006.

Badala yake madaktari walimshauri mwanamke kuenda kwa polisi na hivyo kuifanya mimba kukomaa.

Kadhalika mahakama imeitaka mahakama nyingine kuamua kiwango cha fidia atakacholipwa mwanamke huyo.

Mwenyewe ametaka kulipwa dola 42,000 za kimarekani kugharamia malezi ya mtoto huyo, ingawa amahakama ilitupilia mbali ombi lake.