Rwanda na A.Kusini kusuluhisha mgogoro

Image caption Jaribio la kumuua Kayumba Nyamwasa lilitibuka Afrika Kusini

Rais Jacob Zuma wa Afrika-Kusini na Paul Kagame wa Rwanda wamekubaliana mjini Luanda Angola, kuanzisha mazungumzo ya pamoja ya kumaliza mzozo wao wa kidiplomasia.

Uhusiano kati ya nchi hizo mbili ulianza kuzorota pale Rwanda ilipowafukuza maafisa sita wa ubalozi wa Afrika Kusini, saa chache baada ya Afrika Kusini kuwatimua wanadiplomasia watatu wa Rwanda kuondoka nchini humo karibu wiki tatu zilizopita.

Afrika Kusini ilichukua hatua hiyo baada ya nyumba ya mpinzani mmoja wa Rwanda anayeishi Afrika Kusini Kayumba Nyamwasa kushambiliwa.

Lakini Serikali ya Rwanda ilisema hatua ya kuwatimua maafisa sita wa ubalozi wa Afrika Kusini mjini Kigali ni ya haki na ilizingatia uchokozi ambao ulianzishwa na serikali ya Afrika Kusini yenyewe kwa kufukuza maafisa watatu wa ubalozi wa Rwanda.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Rwanda ilisema kuwa Afrika Kusini ndio ilianza uchokozi kwa kuwatimua mabalozi wake watatu

Jenerali Kayumba Nyamwasa, ambaye aliwahi kuwa mkuu wa majeshi nchini Rwanda, hakuwa nyumbani wakati wa shambulio hilo.

Nyumba yake iliharibiwa huku komputa na baadhi ya nyaraka zilichukuliwa.

Mkutano wa usalama uliofanyika mjini Luanda ulijadili hali kati ya nchi hizo mbili huku viongozi hao wawili wakikikutana ana kwa ana kwa mara ya kwanza tangu mzozo huo kutokea.

Rais Zuma alisema kuwa wamekubaliana kusuluhisha mgogoro huo na pia kupata taarifa ya pamoja ili kuweza kusuluhisha tofauti kati yao.

Kadhalika Rais Zuma aliongeza kwamba serikali yake inatekeleza wajibu wake wa kimataifa kwa kuwapa hifadhi watu wanaoomba. Viongozi hao wawili wamekubaliana kukutana kwa ajili ya kuzungumzia swala hilo baadaye.