Liverpool yarejea kileleni,Uingereza

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Liverpool 4-0 Tottenham Hotspurs

Liverpool imejikita kileleni mwa Jedwali la ligi kuu ya premia baada ya kuinyuka Tottenham hotspurs 4-0 katika mechi iliyokuwa ikisubiriwa na wengi iliyochezwa uwanjani wa Anfield.

Younes Kaboul alijifunga mwenyewe kunako dakika ya pili baada ya pasi ya chini kwa chini kutoka kwa Glen Johnson na kuwapa wenyeji wao kila sababu ya kutabasamu.

Na kutokea hapo Luis Suarez alifanya mambo kuwa 2-0 baada ya Michael Dawson kucheza visivyo.

Philippe Coutinho alitia chumvi kwenye jeraha la Tottenham alipotikisa wavu na bao la tatu, miguu 25 toka langoni.

Jordan Henderson alifunga bao la nne kwa mkwaju wa free-kick

Ushindi huo sasa umeifanya Liverpool kurejea kileleni kwa alama 71 mbili zaidi ya wapinzani wao wa karibu Chelsea .

Reds wanaiongoza Manchester City, kwa alama nne licha ya vijana hao wa Manuel Pellegrin kuwa na mechi mbili zaidi za kucheza .

Hata hivo Man City na Chelsea bado watakabiliana na vijana wa mkufunzi Brendan Rodgers Liverpool katika uga wa Anfield.

Iwapo watashinda mechi hizo basi Liverpool itajiweka katika nafasi nzuri ya kunyakua taji la ligi kuu kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1989-90.

Arsenal ni ya nne kwa alama 64.

Everton iliyosajili ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Fulham inafunga orodha ya tano bora kwa alama 60.