''AKP imeshinda kura Uturuki'' Erdogan

Image caption Recep Tayyip Erdogan atangaza AKP imeshinda uchaguzi wa mabaraza.

Waziri mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ametangaza kuwa chama chake cha Justice and Development Party (AKP) kimeshinda uchaguzi wa mabaraza uliofanyika jumapili kwa kuzoa takriban nusu ya kura zote zilizopigwa .

Matokeo ya awali yanaonesha kuwa Chama cha Justice and Development kilipata asilimia 45 % ya kura karibu asilimia 20% zaidi ya chama kikuu cha upinzani, The CHP.

Mwandishi wa BBC aliyeko Istanbul ,Selin Girit amesema kuwa maafisa wa chama cha AKP tayari wameanza kusheherekea ushindi wa chama chao.

Uchaguzi huu unatumika na wadau kuwa kigezo cha matokeo ya kura za urais zilizoratibiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu.

Kura za ubunge zimeratibiwa kufanyika mwakani.

Image caption Recep Tayyip Erdogan atangaza AKP imeshinda uchaguzi wa mabaraza

Katika mji mkuu, Ankara, kulikuwa na ushindani mkali huku vyama vyote vikidai kushinda.

Uturuki ilishuhudia ghasia mbaya zaidi dhidi ya utawala wa miaka kumi wa bwana Erdogan, katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Aidha waziri huyo mkuu anakabiliwa na tuhuma za ongezeko la visa vya ufisadi dhidi ya utawala wake .

Wengi wa wafuasi wa Erdogan' walipinga madai hayo.

Fauka ya uchaguzi huu kuwa wa amani kwa kiwango kikubwa visa kadha vya mapigano vimeripotiwa kutoka maeneo ya kusini mwa mji wa Hatay na miji mingine Mashariki mwa Uturuki haswa Sanliurfa.

Watu wanane wamefariki kutokana na ghasia hizo.

Image caption Recep Tayyip Erdogan atangaza AKP imeshinda uchaguzi wa mabaraza

Kabla ya uchaguzi huu Waziri Recep Tayyip aligonga vichwa vya habari kote duniani baada ya kufunga mitandao ya kijamii ya Twitter na Youtube kwa madai ya kutumiwa na mahasidi wa serikali yake

kueneza uongo na madai ya ufisadi dhidi yake .

Zaidi ya wapiga kura milioni hamsini walisajiliwa kushiriki kura hii.