Maelfu ya waisilamu wahofia kuuawa CAR

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wanajeshi wanashambuliwa na wapiganaji wa kikrsito wa Anti Balaka

Umoja wa Mataifa unasema hali ya usalama katika mji mkuu wa Jamuhuri ya Afrika ya Kati imeendelea kuzorota, huku taharuki ikiendelea kutanda kati ya walinda amani na wapiganaji wa kikristo Anti -Balaka.

Taarifa zinasema kwamba zaidi ya watu 20 waliuawa na 100 kujeruhiwa hapo Jumamosi wakati wanajeshi wa Chad walipowafyatulia risasi wakaazi wengi ambao ni Wakristo.

Shirika la Umoja huo la kuwahudumia wakimbizi, linasema kuwa maisha ya maelfu ya waisilamu yamo hatarini kwani wengi wanakabiliwa na tisho la kuuawa na wakristo

Shirika hilo linajaribu kuwahamisha wakimbizi 19,000 waisilamu wanaoishi katika vitongoji vinavyozingira mji mkuu Bangui.

Shirika shirika hilo limesema kuwa karibu watu elfu kumi na sita wameachwa bila makao katika siku kumi zilizopita.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Waisilamu wamekimbilia nchi jirani ya Chad kutoroka mauaji

Wengi wametoroka vita vinavyoendelea kupamba moto mjini Bnagui ambako watu sitini waliuawa hivi maajuzi.

Zaidi ya watu 20 kati ya waliofariki waliuawa na wanajeshi wa Chad waliowafyatulia risasi Jumamosi katika mtaa wenye wakristo wengi.

Kwa mujibu wa Umoja huo, wapiganaji wa kikristo wamezidisha mashambulizi dhidi ya waisilamu na walinda amani wa Muungano wa Afrika.

Vurugu zilianza mwezi Machi, baada ya waasi wa Seleka kumwondoa mamlakani Rais mwezi Machi mwaka 2013

Licha ya kupelekwa kwa wanajeshi 6,000 wa muungano wa Afrika pamoja na wanajeshi wengine 2,000 wa Ufaransa, vita vimekuwa vikikithiri