Polisi wategua bomu mtaani Eastleigh

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Polisi wapambana na vurugu mtaani Eastleigh

Maafisa wa utawala nchini Kenya wamepata Bomu moja kubwa karibu na mtaa wa Eastleigh kunakoishi wasomali wengi ingawa wameweza kulitegua.

Maafisa hao kutoka kitengo cha kushughulikia majanga nchini humo walisema kuwa bomu hilo lilipatikana katika eneo la Mlango Kubwa katika barabara ya Juja karibu na Eastleigh.

Mapema leo watu wawili walikamatwa baada ya kupatikana wakiwa na maguruneti mawili nyumbani mwao wakati polisi wakiendelea na msako mkali mtaani Eastleigh.

Wawili hao, Mume na mkewe walikuwa nyumbani wakati polisi walipopata habari kuwahusu na vifaa walivyomiliki.

Mume mwenye umri wa miaka 60 inaarifiwa aliwauzia vijana vilipuzi ambavyo walitumia kwa mashambulizi mjini Mombasa karibu wiki mbili zilizopita.

Polisi wamekuwa wakifanya msako katika mtaa huo wa Easteligh tangu mashambulizi ya maguruneti kuwaua watu 6 Jumatatu usiku na kuwajeruhi wengine 30.

Mkuu wa polisi alisema kuwa wawili hao walikamatwa pamoja na watu wengine 400 katika eneo hilo huku msako wa polisi ukiendelea.

Polisi wanasema kuwa wanawahoji wawili hao kuona ikiwa wanaweza kupata taarifa zaidi

Takriban watu 657 walikamatwa na polisi Jumatatu usiku mtaani Eastleigh, baada ya shambulizi la kigaidi dhidi ya mkahawa kuwaua watu sita.

Kumekuwa na mashambulizi mengine kama hayo mjini Nairobi na Mombasa katika miezi ya hivi karibuni ambayo polisi wanasema yanafanywa na vijana waisilamu wenye itikadi kali za kiisilamu.