Waathiriwa wa Osama kufidiwa Tanzania

Image caption Shambulizi la kigaidi lililotikisa Tanzania mwaka 1998

Watanzania walioathirika na mlipuko wa mabomu katika ubalozi wa Marekani yaliyopangwa na Osama bin Laden mjini Dar es Salaam wameshinda kesi yao na sasa watalipwa fidia.

Katika hukumu iliyotolewa na Jaji wa mahakama kuu ya Marekani Thomas Bates mjini Columbas, familia tisa za watu waliokufa na waliojeruhiwa watalipwa jumla ya dola laki nne na ishirini za Marekani.

Hukumu hii inakuja kufuatia kesi iliyofunguliwa mwaka 2000 kwa msaada wa wanasheria wa kimarekani.

Jaji aliyekuwa anasikiliza kesi hiyo huyo alitoa hukumu ya awali tangu mwaka 2011 na kilichokuwa kimebaki ni utoaji wa fidia hiyo.

Mmoja wa waathirika hao Judith Mwila ambaye mume wake alifariki katika mkasa huo, amezungumza na mwandishi wa BBC Baruan Muhuza mjini Dar es salaam na kusema kuwa yeye amepata taarifa hiyo kupitia kwenye gazeti tu.

Msimamizi wa waathirika hawa Fuad Latif ambaye ni kiungo kati yao na mawakili wanaoendesha kesi hiyo, ameiambia BBC kuwa Mahakama hiyo inaandaa utaratibu wa kukamata baadhi ya mali za serikali ya Iran na Sudan kwa ajili ya kulipia fidia hiyo.

Nchi hizo zinadaiwa kuhusika na mipango ya kukamilisha milipuko hiyo kwa kumsaidia Osama bin Laden kutekeleza ukatili huo kwa kutumia kundi lake la Al Qaida.

Watu kumi walikufa katika kadhia hiyo ya ubalozi wa Marekani mjini Dar es Salaam mwaka 1998.

Kijana Mtanzania Ahmed Ghailani anatumikia kifungo cha maisha jela nchini Marekani baada ya kukutwa na hatia ya kupanga mashambulizi katika balozi za Marekani mjini Nairobi na Dar es Salaam.