'Condom' za kuwavutia vijana A. Kusini

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Vijana wanakosa kutumia Condom za kawaida kwa sababu haziwavutii

Serikali ya Afrika Kusini imeanza mpango wa kuwapa vijana wa shule za sekondari kuendelea juu mipira ya Condom zenye rangi tofauti tofauti na ambazo zina harufu nzuri ya kuvutia.

Mpango huu unalenga kuzuia wanafunzi kuchoka kutumia mipira ya kawaida ya condom wanaposhiriki ngono.

Waziri wa afya Aaron Motsoaledi, ameyasema hayo baada ya utafiti uliofanywa nchini humo kuonyesha kuwa matumizi ya mipira ya Condom imepungua nchini Afrika Kusini.

Inaarifiwa kinachosababisha upungufu huo ni kwamba Condom za kawaida zinazotolewa na serikali hazina mvuto wowote kwa vijana.

Afrika Kusini ina watu milioni 6.4 wanaoishi na virusi vya HIV, idadi hiyo ikiwa juu zaidi kuliko nchi yoyote duniani.

Utafiti uliofanywa na kitengo cha serikali cha utafiti wa afya, ulionyesha maambukizi yameongezeka hadi asilimia 12.2.

Takriban watu milioni 2 hupata matibabu ya ARV's au madawa ya kupunguza makali ya HIV.

Hata hivyo baadhi ya mashirika ya misadaa yanaonya kuwa baadhi ya kliniki zinakabiliwa na upungufu wa dawa hizo.

Condom hizo zitatolewa na serikali kwa vijana bila malipo.