84 wafariki kutokana na Ebola Guinea

Haki miliki ya picha
Image caption Wataalamu wa afya wanapambana vilivyo na ugonjwa huo kuudhibiti katika kanda ya Afrika Magharibi

Wataalamu wa afya nchini Guinea wamesema kuwa Watu themanini na wanne wamefariki kutokana na ugonjwa hatari wa Ebola.

Wakati huo huo watu saba wamethibitishwa kuugua ungonjwa huo katika nchi jirani ya Liberia.

Sierra Leone na Gambia pia inakisiwa kuwa kuna watu wanaougua ugonjwa huo.

Firmin Bogon ambaye ni raia wa Guinea aliieleza BBC kuwa jamaa wake kumi walifariki kutokana na ugonjwa wa Ebola.

Alisema dada yake aliyekuwa wa kwanza kufariki kutokana na ugonjwa huo, aliwaambukiza watu wengi katika kijiji chake walipo ibeba maiti yake kuizika.

Nchi jirani ya senegal imefunga mipaka yake na Guinea kufuatia kuzuka kwa ugonjwa huo hali ambayo imewaacha madereva wengi wa lori wanaopeleka bidhaa nchini humo kukwama njiani.

Wakati huo huo makampuni kadhaa ya madini ya kigeni yamewaondoa baadhi ya wafanyakazi wao wa kimataifa kutoka Guinea.